ROONEY KUIKABILI GOR MAHIA
NA MARIMU MTORO
Mshambuliaji Wayne Rooney atacheza mechi yake ya kwanza akiwa na kikosi cha Everton leo dhidi ya Gor Mahia kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (saa 11:00 jioni).
Rooney atacheza mechi hiyo ya kwanza tangu alipoiacha klabu hiyo ya Merseyside mwaka 2004, pia winga Aaron Lennon atacheza mchezo huo baada ya kupona ugonjwa wake wa msongo wa mawazo.
Rooney atakiongoza kikosi hicho cha kocha Ronald Koeman kuhakisha kinatoka na ushindi dhidi ya Gor Mahia mabingwa wa Kombe la SportPesa.
Rooney amepokelewa kwa shangwa tangu alipoamua kurejea Goodison Park na atacheza mechi hiyo ya kwanza akiwa na jezi ya Blues tangu alipofanya hivyo Mei 2004.
Nahodha huyo wa zamani wa England, alifanya mazoezi na kikosi hicho jana Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa.
Pamoja na mashabiki wa Afrika Mashariki kuwa na wasiwasi kwamba Gor Mahia itachapwa mabao mengi, wenyewe wamesema watawaduwaza wengi.
Beki wa Gor Mahia, Harun Shakava amesema wanauchukulia mchezo huo kama michezo mingine na kwamba wamekuja kwa ajili ya kupambana.
“Kila mtu ana ari ya kutosha. Ni mechi ya kihistoria kila mchezaji anatamani kucheza dhidi ya timu ya Ligi Kuu England," anasema Shakava.
Winga Oliver Maloba alisema tamaa yake kubwa ni kuwapiga chenga masupastaa wa Everton. Natambua uwezo binafsi nilionao. Vile vile suala la kumchenga mtu kama Rose Barkley itanipa raha.”

Comments
Post a Comment