LIPULI LAZIMA IZIKWE
Katika mchezo huo Yanga itawakosa nyota wake Obrey Chirwa na Pius Buswita kutokana na kesi tofauti ambapo Buswita amesimamishwa mwaka mmoja baada ya kubainika kusaini mara mbili Simba na Yanga.
Chirwa licha ya kuwa ni majeruhi lakini pia, alisimamishwa na Kamati ya usimamizi ya uendeshaji Bodi ya ligi ile ya masaa 72 ya msimu uliopita baada ya kumpiga mwamuzi Ludovic Charles katika mchezo wa kumaliza msimu dhidi ya Mbao FC hivyo, anasubiri suala lake kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Yanga imekuwa haitabiriki katika mechi zake za mwanzo kuna wakati huanza vibaya na wakati mwingine huanza vyema, lakini mara nyingi imekuwa ikifanya vizuri katika mechi za nyumbani.
Lipuli ni timu ngeni kwenye ligi ya msimu huu lakini faida waliyokuwa nayo ni kufundishwa na kocha mzoefu Seleman Matola, ambaye anaifahamu Yanga vizuri. hivyo hautakuwa mchezo rahisi kwa kila mmoja ingawa Yanga inapewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na aina ya kikosi ilichosajili msimu huu.
Baadhi ya nyota wa Yanga waliong’ara katika mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Simba hivi karibuni, Ibrahim Ajib, Donald Ngoma, Gadiel Michael, Thaban Kamusoko na Papy Kabamba Tshishimbi wanatarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha kocha George Lwandamina akitafuta ushindi wake wa kwanza ili kutetea taji hilo wanalolishikilia mara tatu mfululizo.
Lakini sio mchezo wa kudharaukwani Lipuli FC licha ya kuwa na kocha mzoefu lakini pia wanajua wanakutana na timu ya aina gani hivyo, watacheza kwa juhudi ili kuhakikisha wanapata ushindi au angalau sare mbele ya mabingwa hao watetezi.
Kocha Lwandamina amesema maandalizi yanakwenda vizuri na wamejipanga kuhakikisha pointi tatu zinabakia kwao.
Amesema kinachotakiwa kwa wachezaji wake ni kujituma na kuanza vyema michuano hiyo.
Kocha Selemani Matola amesema Yanga ni timu kubwa na nzuri hivyo, anaamini mchezo hautakuwa rahisi kwao.
Amesema wamefanya maandalizi ya kutosha watahakikisha wanapambana na kupata pointi tatu.
Comments
Post a Comment